Serikali imesema kuwa, itaendelea kuwakaribisha Wawekezaji kwenye sekta ya Mafuta na Gesi ikiwa ni eneo ambalo linapigiwa chapuo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na hasa ukuaji wa Viwanda.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, – Angella Kairuki ametoa kauli hiyo wakati akimuwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ufunguzi wa Kongamano la Tatu la Wadau wa Mafuta na Gesi linaofanyika jijini Dar es salaam.
Waziri Kairuki amesema kuwa, mpango wa uboreshaji mazingira ya biashara na uwekezaji (Blue Print) umeanisha maeneo yote ya Mafuta na Gesi kama ni muhimu katika ukuaji wa Uchumi wa Taifa.
Ameongeza kuwa, Serikali ipo katika mchakato wa uandaaji wa sheria ya Uwekezaji itakayoainisha mazingira na maeneo ambayo yanapewa kipaumbele katika uwekezaji na uboreshaji wa biashara hapa nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amesema kuwa, Tanzania ina utajiri mkubwa wa Mafuta na Gesi, na hivyo kuwataka Wawekezaji wenye nia ya kufanya biashara waangalie namna wanavyoweza kuzitumia rasilimali hizo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Dkt Kalemani amesema kuwa, mbali na Gesi lakini pia Tanzania ina uwezekano mkubwa wa kugundua mafuta ambayo ni nishati muhimu kwa maendelea ya Taifa, na hivyo kuzitaka Kampuni mbalimbali kujitokeza kuwekeza katika sekta hiyo.
Awali Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, – Salma Abood Talib alisema kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafanya jitihada za kuhakikisha sekta za Mafuta na Gesi zinakuwa na manufaa kwa Wakazi wote wa Zanzibar.
Akitoa maelezo kuhusu kongamano hilo la Tatu la Wadau wa Mafuta na Gesi linaofanyika hapa nchini mwaka huu, Kaimu Mwenyekiti wa Shirikisho la watoa huduma za Mafuta na Gesi nchini Abdulsamd Abdulrahim amesema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la Washiriki katika kongamano hilo tangu lilipoanzishwa mwaka 2017 na hiyo inatoa picha kwamba sekta hiyo inakuwa kila mwaka.
Abdulrahim ameipongeza serikali kwa namna inavyoweka mazingira mazuri ya uwekezaji, kulinda rasilimali za asili na kukuza uchumi wa Taifa.