Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo.
Dkt Shein ametoa wito huo jijini Tanga, wakati wa kumbukumbu ya miaka 19 ya kifo cha Baba wa Taifa, Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na hitimisho la wiki ya Vijana Kitaifa.
Amesema kuwa Hayati Mwalimu Nyerere alikua anajali na kusisitiza umoja siku zote za maisha yake, hivyo ni vema Watanzania wakaendeleza umoja huo ili Taifa liweze kupata maendeleo kwa haraka.
Kuhusu rushwa, Dkt Shein ametoa wito kwa Watanzania wote bila kujali tofauti zao, kupiga vita vitendo vya rushwa kwa kutoa
taarifa za watu wanaojihusisha na vitendo hivyo ili kumuenzi Baba wa Taifa ambaye aliichukia rushwa.
Kwa upande wa Mwenge wa Uhuru, Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesisitiza kuwa serikali zote mbili zitaendelea kuzienzi na kuzithamini mbio za Mwenge wa Uhuru.
Amewataka wale wote ambao wamekua wakiubeza Mwenge huo wa Uhuru waache mara moja kwa kuwa umekua ukihamasisha uendelezaji wa miradi mbalimbali nchini kote.
Akizungumzia wiki ya vijana Kitaifa, Dkt Shein amesema kuwa imekua na manufaa makubwa kwa kutoa mafunzo ya aina mbalimbali kwa vijana.
Amewataka vijana nchini kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo na kujiepusha na vitendo viovu ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.