Serikali kuendelea kushirikiana na sekta binafsi

0
2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali inathamini uwepo wa sekta binafsi nchini na kwamba inaendelea kushirikiana nayo.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam alipokutana na bodi mpya ya Taasisi ya Sekta Binafsi nchini, ambayo ilikwenda kujitambulisha.

Amempongeza Mwenyekiti wa taasisi hiyo Salum Shamte na wajumbe wa bodi hiyo mpya kwa kuchaguliwa kuingoza taasisi hiyo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

“Serikai inadhamira ya dhati ya kushirikiana na taasisi hii kwa sababu ndio muwezeshaji wa kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025,” amesema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya Sekta Binafsi Nchini Salum Shamte amesema kuwa sekta hiyo inatambua juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya biashara nchini.

“Sisi tupo tayari kushirikiana na serikali kwa kuwabana wafanyabiashara ambao wanaenda kinyume na maadili na sheria, ila tunaomba serikali ishirikiane nasi katika utekelezaji wake,”ameongeza Shamte.

Pia ameiomba serikali iendelee kutoa vivutio kwa biashara zinazoanza ili kuhamasisha uwekezaji kwa kuwa baadhi yake zimeonesha gharama kubwa za uzalishaji.