Serikali kuendelea kumkumbuka Dkt Mengi

0
597

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali  itaendelea kumkumbuka Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, –  Marehemu Dkt Reginald Mengi kwa moyo wake wa kujitoa na kuwasaidia wengine.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo mkoani Kilimanjaro wakati wa Ibada ya mazishi ya Dkt Mengi iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania – KKKT Moshi Mjini.

Akitoa salamu za serikali, Waziri Mkuu  Majaliwa amesema kuwa Marehemu Dkt Mengi alitumia muda wake mwingi pamoja na mali zake nyingi kuwasaidia watu wenye uhitaji hasa wale wenye ulemavu.

Amesema kuwa wakati wote Marehemu Dkt Mengi alikua yupo tayari kupokea mawazo na ushauri ambao aliamini kuwa ungemuwezesha kutimiza azma yake ya kuwasaidia watu wenye ulemavu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, serikali pia itaendelea kumkumbuka na kumuenzi Marehemu Dkt Mengi kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Taifa kupitia uwekezaji mkubwa alioufanya.