Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwepo kwa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF), ni njia mojawapo ya kuukuza na kuutangaza utalii pamoja na urithi wa Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu jijini Zanzibar, alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa ZIFF, ukiongozwa na Mkurugenzi wake Profesa Martin Muhando.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na ZIFF ambazo amesisitiza kwamba ndio njia muhimu ya kuukuza na kuutangaza utalii wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwinyi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha tamasha hilo la ZIFF linaendelea kupata mafanikio zaidi.