Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa Afya nchini kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anatoa kibali cha kuajiri watumishi wapya katika Sekta ya Afya kila Mwaka.
Hayo ameyasema Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Momba wakati akiendelea na ziara yake ya siku Tatu katika Mkoa huo.
“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujali Sekta ya Afya ambapo anatoa kibali kila Mwaka cha ajira mpya Kwa hiyo tutaendelea kuajiri lakini pia kutumia wadau wa maendeleo kuleta wataalamu hususan wa Maabara”. Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema kufuatia changamoto hiyo ya uhaba wa watumishi katika Hospitali ya Wilaya ya Momba ni kutokana na kuongezeka kwa vituo vya Afya ambapo awali kulikua na vituo vya Afya Viwili na Sasa kuna Vituo vya Afya Vitano.
Aidha, Waziri Ummy amewataka watumishi wa Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Momba kuhakikisha wanaendelea kufanya kazi kwa kufuata misingi ya Taaluma yao, weledi na maadili ili wananchi kuendelea kupata huduma bora.
“Muda wote tapohudumia wagonjwa tuzingatie weledi na Taaluma zetu na la pili tuzingatie maadili ya Taaluma yetu na la Tatu tuzingatie viapo vyetu kwa kuwa kazi yetu ni kuokoa maisha ya watu”. Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy Mwalimu yupo katika Mkoa wa Songwe kwa ziara ya siku Tatu kwa lengo la kukagua huduma zinazotolewa katika Hospitali a Wilaya, vituo vya Afya pamoja na Zahanati, pia upatikanaji wa dawa na utolewaji wa chanjo.