Serikali kuboresha miundombinu ya Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro

0
130

Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara zinazotumika kupeleka watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro kwa kushirikiana na wadau na mamlaka zinazohusika, kwa lengo la kuwawezesha watalii wanaotembelea hifadhi hiyo kufika kwa urahisi.

Hayo yamesemwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuboresha barabara zote zinazowapeleka watalii mlima Kilimanjaro.

Amefafanua kuwa miongoni mwa jitihada zilizofanyika za kuboresha miundombinu ya barabara katika hifadhi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara za Machame, Mweka na Marangu kwa kiwango cha lami.

Pia amesema Serikali imeendelea kufanya ukarabati wa mara kwa mara wa barabara za changarawe zinazoelekea katika lango la Rongai, Lemosho, Kilema, Londorosi na Umbwe.