Serikali kuboresha maslahi ya Wanahabari

0
156

Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi ametoa rai kwa wadau wote wa habari kushirikiana kutafuta suluhu za changamoto za kiuchumi zinazovikabili vyombo vya habari nchini.

Dkt. Abbasi ametoa rai hiyo mkoani Dar es salaam wakati wa semina iliyowashirikisha Waandishi wa habari, iliyoandaliwa kwa pamoja na wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Miongoni mwa malengo ya semina hiyo ni kutoa mapendekezo ya namna gani vyombo vya habari nchini viimarishe mapato na uchumi wao.

“Mara chache sana tunapofanya semina na makongamano tunakumbuka kutathmini hili kwamba uhuru wa kiuchumi wa Wanahabari ni muhimu sana, Mwanahabari ambaye analipwa kiduchu, hana uhakika wa mshahara, hana bima, hana pensheni kabla hajaenda kutafuta stori tayari hana uhuru,” amesema Dkt. Abbasi.

Amewataka Wadau hao wa habari kutoa mapendekezo yao, ili Serikali nayo ione itafanya nini katika sekta ya habari.

“Leteni mawazo makini ili kile sisi Serikali tunachopaswa kufanya tukifanye, na kinachopaswa kuanzia kwa wadau wa sekta wenyewe kianzishwe,” amesisitiza Dkt. Abbasi.

Wakati wa semina hiyo, Dkt. Abbasi pia ametoa tuzo kwa Waandishi wa Habari na wadau wa habari Wanawake waliotoa mchango mkubwa katika sekta hiyo ambao ni Edda Sanga, Penzi Nyamngumi na Joyce Kiria.

Semina hiyo ni maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Uhuru wa vyombo vya habari duniani, yatakayofanyika jijini Arusha Mei 3 mwaka huu.