Serikali kuajiri walimu 6,000

0
189

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ina mpango wa kuajiri walimu 6,000 ili kuwezesha shule zote nchini kuondokana na changamoto ya walimu.

Rais ameyasema hayo katika siku yake ya kuzaliwa alipokuwa akizungumza kwa njia ya simu na walimu pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

“Kwa ujumla mambo ndani ya sekta ya elimu ni mengi mno, kuna ujenzi wa miundombinu, kuna kutoa vifaa vya kusomeshea, kuna kujenga mazingira ya uwezeshaji kwa ujumla, lakini baada ya kujenga madarasa na kuyawekea ‘furniture’ [samani], kinachofuata ni kuongeza ajira ya walimu, nitaongeza walimu 6,000 au 7,000 hivi tutawaongeza na kuwasambaza ili waendane na ujengaji wa madarasa,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa anafahamu kuwa changamoto ipo katika shule za msingi, hivyo ataendelea kuboresha miundombinu ya shule za msingi ikiwemo kuongeza madarasa na samani.

“Changamoto ipo kwenye shule za msingi, tulianza kuweka katika fedha hizi za UVIKO19 ambapo tumewekeza vizuri sana kwenye shule shirikishi, lakini pia mnajua kwamba kuna fedha za tozo ambazo tunazikusanya kila mwezi na tunaendelea kujenga madarasa katika ngazi za msingi,” ameongeza Rais Samia Suluhu Hassan.