Serikali inafanya majadiliano kuhusu hali ya Ngorongoro

0
220

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika mkutano kuhusu hali ya Hifadhi ya Ngorongoro na tayari utekelezaji umeanza.

Ameeleeza kuwa tayari amekutana na wizara ya Maliasili na Utalii, uongozi wa mkoa na wadau, na hatua inayofuata ni kuzungumza na wananchi.

Aidha, ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya semina ya kuwaelimisha wabunge wote wajue nini kilikuwepo Ngorongoro na nini hakipo, ili wakati wanapinga au kukubali hoja zitakazotekelezwa wafanye hivyo wakiwa na uelewa.

Waziri Mkuu amesema hayo kufutia ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuonesha kuwa idadi ya watu na mifugo imeelendelea kuongezeka kwenye eneo hilo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Baadhi ya wabunge wameshauri wananchi na mifugo iliyomo kwenye eneo hilo iondolewe, huku wengine wakishauri kuwa maboresho yafanyike wananchi wakiendelea kuwemo ndani ya hifadhi kwani wamekuwa mstari wa mbele kulinda mazingira na wanyama.