Serikali imedhamiria kuendesha sekta ya sanaa kibiashara

0
151

Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuendesha sekta ya sanaa kibiashara na kuongeza tija ikiwa ni pamoja na kuwezesha sekta hii kutumika kama nyenzo ya kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Sekta ya Sanaa 2021 ambao lengo lake ni kujadili kwa pamoja masuala yanayohusu sekta ya sanaa kati ya Serikali na wadau ili kufikia lengo la kuifanya sekta hii kuendeshwa kibiashara.

“Serikali imejipanga kuweka mazingira wezeshi ya kukuza sanaa zetu ili kufikia viwango vya kimataifa na kuboresha mbinu na mikakati ya utekelezaji wa sera na sheria za kuimarisha kazi za sanaa nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sanaa hususani wasanii,” amaeeleza Naibu waziri Kigahe.

Aidha, Exaud Kigahe ameeleza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara ni mdau mkubwa wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kwani Sekta ya Sanaa ni kiwanda kinachozalisha bidhaa na huduma za sanaa ambazo zinahitaji mchango mkubwa wa Wizara ya Viwanda na Biashara katika kuweka sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya kusimamia uendeshaji wake na kuiendeleza kama inavyofanyika katika sekta nyingine za kiuchumi hapa nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaaa wa Wizara ya, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Ishengoma ameeleza kuwa ili kuendesha sanaa kibiashara, serikali imeanzisha mfuko wa utamaduni na sanaa ambao utasaidia kuimarisha sekta hiyo kwa kudhamini mafunzo vilevile kutoa mkopo kwa masharti nafuu ya kusaidia sanaa na utamaduni na mpaka sasa serikali imeshatoa bilioni moja na milioni mia tano za kuwezesha mfuko huo.