Serikali: Hakuna uhaba wa mafuta nchini

0
267

Waziri wa Nishati January Makamba amesema kuwa mafuta yaliyopo kwenye maghala, vituo vya mafuta pamoja na yale yanayoshushwa bandarini kwenye meli yanatosheleza mahitaji ya mafuta nchini.

Waziri Makamba ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi ya Wizara jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwatoa hofu wananchi kufuatia ongezeko la bei za mafuta lililotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) jana.

“Hakuna uhaba wa mafuta nchini na hivyo hakuna haja kuwepo kwa taharuki juu ya malighafi hiyo. Mfumo wetu wa uagizaji na uingizaji mafuta ni mfumo thabiti ambao unatuhakikishia usalama wa mafuta nchini,” ameeleza.

Waziri Makamba ameongeza kuwa hadi kufikia Aprili 1, 2022 petroli iliyokuwa kwenye maghala ni jumla ya lita 118,594,024 yanayotosheleza siku 27, dizeli lita 116,486,705 yanatosheleza siku 19, mafuta ya taa lita 6,823,710 yanatosheleza siku 108 na mafuta ya ndege lita 12,841,822 yanatosheleza siku 35.

Vilevile kuna meli ambazo zimewasili nchini na zinaendelea kushusha mafuta zikiwa na lita 86,256,000 za dizeli. Hivyo kwa kuzingatia mafuta yaliyokuwepo tarehe 01 Aprili 2022 nchi itakuwa na jumla ya lita 202,742,705 za mafuta ya dizeli zitakazotosheleza matumizi ya nchi kwa siku 33.