Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameeleza kuwa uchumi wa taifa umeendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2019, ukuaji halisi wa Pato la Taifa (GDP) ulifikia asilimia 6.9.
Majaliwa ameyasema hayo bungeni mjini Dodoma alipokuwa akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya waziri mkuu na ofisi ya bunge kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Katika hotuba hiyo Majaliwa alizitaja baadhi ya shughuli zilizochangia ukuaji huo kwa viwango vikubwa ni pamoja na ujenzi asilimia 14.8, uchimbaji wa madini na mawe asilimia 12.8, habari na mawasiliano asilimia 11.0, uchukuzi na uhifadhi wa mizigo asilimia 8.8 na huduma za usambazaji maji asilimia 8.5.
Kuhusu mfumuko wa bei amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2019 hadi Januari 2020, mfumuko wa bei ulikuwa wastani wa asilimia 3.7. Ameongeza kuwa wastani huo ni chini ya lengo la taifa la kipindi cha muda wa kati la asilimia 5.0, na chini ya malengo ya asilimia 7.0 kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na asilimia 8.0 kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika Mwaka 2020/2021, amesem serikali itaendelea kuimarisha sekta za uzalishaji na utoaji huduma ili kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa.