Watanzania wametakiwa kuchangamkia fursa za kibiashara kwenye mradi wa kusindika gesi asilia (LNG) unaotarajiwa kuzalisha ajira nyingi kwa wazawa mkoani Lindi.
Akizungumza mara baada ya kukagua eneo la mradi, Mwenyekiti wa timu ya Serikali ya majadiliano ya mradi wa LNG Charles Sangweni amesema, mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa na utakuwa ukisindika gesi asilia ambayo itauzwa ndani na nje ya nchi.
Amewasisitiza Watanzania kuanza kuchangamkia fursa za uwekezaji wakati wa ujenzi pamoja na uendeshaji wa mradi huo.
Kwa mujibu wa Sangweni, timu yake imejipanga kusimamia kikamilifu maslahi ya Taifa wakati wa kufikia makubaliano ya uendeshaji wa mradi huo mkubwa utakaochochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Mjumbe wa timu ya Serikali ya majadiliano katika mradi huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. Elias Mwashiuya amesema, timu hiyo imejipanga kusimamia kikamilifu maslahi ya Taifa katika makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo wa kusindika gesi asilia.
“Timu hii imejipanga vizuri kwa masuala ya kisheria, na kwamba baada ya majadiliano haya kukamilika tunategemea kupata mkataba hodhi utakaosaidia kuruhusu mikataba midogo midogo itakayorahisisha utekelezaji mradi huu kwa maslahi mapana ya Taifa.” amesema Dkt. Mwashiuya
Naye Katibu Tawala wa mkoa wa Lindi, Rehema Madenge amesema, hatua ya timu hiyo kwenda mkoani humo kukagua eneo utakapojengwa mradi wa kusindika gesi asilia imefufua matumaini kuwa mradi uko mbioni kuanza.
Amesema tayari Vijana wa mkoa wa Lindi wameanza kupata mafunzo mbalimbali katika Chuo cha Ufundi – VETA na pia Wananchi wameanza kuhamasishwa kuchangamkia fursa za kibiashara kwenye mradi huo.
Mradi wa kusimdika gesi asilia ni mradi wa kimkakati unaotekelezwa na Serikali na unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa Taifa ikiwa ni pamoja na kuzalisha ajira nyingi.