Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania anayekipiga katika klabu ya Fenérbahce ya Uturuki, Mbwana Samatta anatarajia kuwasili nchini kesho kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi.
Mchezo huo uliopo kwenye kalenda ya FIFA utakapigwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam Oktoba 11 mwaka huu.
Samatta anarejea nchini akiwa ameanza vizuri kibarua chake huko Uturuki baada ya kufungia timu yake magoli mawili na kuipatia ushindi wa 2-1 dhidi ya Fatih Karagümrük S.K, ukiwa ni mchezo wake wa kwanza na timu ya Fenérbahce.
Taifa Stars inaingia kambini leo Oktoba 5 ambapo mbali na Samatta wachezaji wengine wa kimataifa walioitwa ni Thomas Ulimwengu, anayetarajiwa kuwasili leo akitokea Congo DR, Himid Mao, Simon Msuva na Nickson Kibabage kutokea Misri na Morocco ambao watawasili Jumatano na Ally Msengi ambaye amewasili akitokea Afrika Kusini.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amesema kuwa wana imani ya kupata matokeo chanya kwenye mchezo huo.
“Tupo vizuri na imani ni kwamba tutafanya vizuri kwa kuwa wachezaji ambao wapo kwenye kikosi wana uzoefu mkubwa na wanajua kutimiza majukumu yao.”
