Nahodha wa timu ya Taifa ya Soka (Taifa Stars),- Mbwana Samatta amejibu shutuma kali zilizoelekezwa kwake na baadhi ya mashabiki wakidai kuwa, alicheza chini ya kiwango katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Libya.
Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter Samatta amesema kuwa, amepokea ujumbe kutoka kwa watu kadhaa ambao wamemweleza kuwa hawajaelewa kiwango alichoonesha katika mechi za timu ya Taifa.
Hata hivyo nahodha huyo wa Stars amesema kuwa, amefurahi kuona watu wanasema ukweli na yeye anatumia maneno hayo ya watu kama chachu ya kujituma zaidi ili aweze kuwa bora zaidi na kumaliza kwa kusema ‘haina kufeli’.
Usiku wa Jumanne, Taifa Stars ilipoteza mchezo wake wa kuwania kufuzu kwa fainali za AFCON mwaka 2021 baada ya kufungwa mabao Mawili kwa Moja na Libya, mchezo uliochezwa nchini Tunisia, kitendo kilichosababisha baadhi ya mashabiki wa Soka nchini kumshukia vikali Samatta kuwa alicheza hovyo.
Mpaka sasa Tunisia inaendelea kukaa kileleni mwa kundi J ikiwa imejikusanyia alama Sita baada ya kushinda mechi zake Mbili, Libya ikifuatia ikiwa inashika nafasi ya Pili ikiwa na alama Tatu sawa na Tanzania na Guinea ya Ikweta inaburuza mkia.
