Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ametoa muda wa saa tano kwa kila halmashauri nchini kutenga sehemu maalum kwa ajili ya kuwekwa washukiwa wa virusi vya corona na kufanya utaratibu wa uchunguzi na kutoa taarifa haraka wizarani.
Waziri Ummy Mwalimu ametoa muda huo jijini Dar es salaam wakati akifungua mafunzo kwa viongozi wa dini nchini, ya namna ya kuepuka maambukizi ya virusi vya corona ambavyo vinazidi kusambaa katika nchi mbalimbali duniani.
“Ninatoa muda mpaka saa 10 jioni hii leo vituo vyote vya afya vya umma nchini viwe vimetenga sehemu maalum ya kuweka mshukiwa wa virusi vya corona na kuripoti haraka iwezekanavyo katika wizara ya Afya kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki”, amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema mpaka sasa Tanzania ni salama na hakuna mgonjwa wa corona, lakini serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kudhibiti ugonjwa huo usiingie nchini ikiwa ni pamoja na kushirikisha taasisi mbalimbali za dini.
“Tunawaomba viongozi wa dini muende mkatoe elimu kwa waumini wenu kuchukua tahadhari kwa kuzingatia kanuni za usafi na pia kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua ambaye ana historia ya kusafiri nje ya nchi”, amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Aidha, ametoa maelekezo kwa taasisi za dini, taasisi za umma, maofisi na shule za serikali na binafsi kuweka sehemu maalum ya kunawa mikono kwa maji yenye dawa ya kuua bakteria ili kuepuka maambukizi yatokanayo na bakteria.
