Ruzuku kupunguzwa katika mpango wa kunusuru kaya masikini

0
241

Serikali imesema kuwa katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), inakusudia kupunguza kiasi cha ruzuku kutoka asilimia 67 hadi 38.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Rais John Magufuli wakati wa hafla ya uzinduzi wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na TASAF na kuongeza kuwa, ruzuku hiyo itatolewa kwa wazee wasiojiweza, watoto wadogo na kwa watu wenye kiwango kikubwa cha ulemavu.

Rais Magufuli amesema kuwa, Serikali imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kasoro na changamoto kadhaa zilizojitokeza awali.

“Awamu hii mpya tumepanga kuitekeleza katika halmashauri zote 185 na Wilaya 11 za Zanzibar na asilimia 60 ya fedha, sawa na shilingi trilioni 1.22 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo takribani Elfu 30 kwenye vijiji na mitaa 16,596 Tanzania Bara na shehia 388 kule Zanzibar’’ amesema Rais Magufuli.

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ile ya sekta ya afya, elimu, maji, barabara na mazingira ambapo katika kutekeleza miradi hiyo kipaumbele kitatolewa kutoka kwa watu wenye nguvu wanaotoka kwenye kaya maskini na kwamba Serikali inatarajia kuzalisha ajira na kuwapatia ujuzi pamoja na stadi za kazi watu milioni 1.2.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Mkuchika amesema kuwa,  katika kipindi cha pili cha awamu ya Tatu ya TASAF, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa changamoto zote zilizojitokeza katika awamu ya kwanza zinapatiwa ufumbuzi ikiwemo kufikia asilimia 30 ya kaya zilizobaki katika maeneo yote nchini.