Rufaa za wagonjwa Mafia kwenda Dar zapungua

0
241

Bohari ya Dawa (MSD) imesema usambazaji wa dawa na vifaa vya kisasa katika Kisiwa cha Mafia mkoani Pwani umesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kutoka kisiwani humo kwenda kutibiwa mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza kisiwani Mafia Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, Diana Kimario amesema, bohari hiyo imefanikiwa kupunguza rufaa hizo za wagonjwa baada ya kufungwa kwa vifaa tiba vya kisasa hususani vya maabara na upasuaji.

“Wilaya hii ina vituo vya afya 25 ambapo vituo 21 vipo Mafia na vituo vinne vipo katika visiwa vidogo ambapo vifaa vilivyosambazwa na MSD vitafanikisha kupunguza changamoto ya rufaa kwa wagonjwa waliokuwa wakisafirishwa kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya huduma,”amesema Diana.

Naye Mganga mkuu wa wilaya ya Mafia Dkt. Maulid Majala amesema hospitali ya wilaya hiyo imepokea zaidi ya shilingi Milioni 550 kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya mawili na shilingi Bilioni 1.39 kwa ajili ya vifaa tiba.

Ametoa wito kwa Watumishi wa hospitali hiyo kuhakikisha uwekezaji huo unaendana na thamani ya huduma zinazotolewa.

Dkt. Majala ameongeza kuwa ujenzi wa majengo hayo na vifaa vya kisasa ni muhimu, kwa kuwa awali walikuwa wakikutana na wagonjwa wa dharura hasa wa ajali na kulazimika kuwapa rufaa kutokana na hospitali hiyo kukosa vitendea kazi.