Rorya yalia na ukatili unaofanywa na wanaume

0
255

Mkuu wa wilaya ya Rorya mkoani Mara, Juma Chikoka amewataka wanaume wilayani humo kutotumia wivu wa mapenzi kama chanzo cha ukatili.

Chikoka ameyasema hayo alipofika kumjulia hali Maria Mwita aliyelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara, anayedaiwa kukatwa mkono na titi na mtu aliyetajwa kuwa ni mume wake.

Chikoka amesema wanaume wengi wilayani Rorya wamekuwa wakitumia wivu wa mapenzi kama chanzo cha ukatili kwa wanawake, na hivyo kuwataka kuacha mara moja tabia hiyo.

Amesema kama binadamu wivu ni kawaida, lakini ni vema akautawala kuliko kuruhusu usababishe madhara makubwa.

Chikoka ameongeza kuwa yapo matukio kadhaa ambayo yamekuwa yakiripotiwa yatokanayo na wivu wa mapenzi, ambapo mbali na kusababisha madhara makubwa lakini pia yamekuwa yakivunja haki za binadamu.

Aidha mkuu huyo wa wilaya ya Rorya amesema, uongozi wa wilaya hiyo kwa kushirikiana na jeshi la polisi wanaendelea na jitihada za kumtafuta mume wa mwanamke huyo ambaye amekimbia mara baada ya kufanya ukatili huo.