Redio Jamii 93.7 FM kupasua anga

0
140

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile amelitaka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kurusha matangazo yenye maudhui yanayojibu matatizo na changamoto zinazoikabili jamii hasa janga la corona.

Akizungumza jijini Dodoma katika hafla ya makabidhiano na uzinduzi wa studio za Redio Jamii 93.7 FM Dodoma inayomilikiwa na TBC, Dkt. Ndugulile amesema hatua hiyo itasaidia kuwasilisha maagizo ya Serikali kwa jamii bila kupotoshwa. 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul amesema, Serikali itaendelea kuiwezesha TBC ili iweze kuboresha matangazo yake ambayo yamebeba maudhui yanayoakisi matakwa ya umma hasa azma ya Serikali ya kuwaletea  maendeleo Wananchi wake.

Naibu Waziri Gekul ametoa wito kwa TBC na vyombo vingine vya Habari nchini kuzingatia weledi na kurusha maudhui yasiyopotosha jamii, ambayo yatawahamasisha Wananchi kufanya kazi kwa bidii, kuwa wazalendo na wenye kuzingatia ustawi mzuri wa Taifa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema, studio hizo za Redio Jamii  93.7 FM Dodoma ni muhimu kwa Wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kati na kwamba itatoa fursa ya kukuza vipaji vya wasanii.