REA na TANESCO watakiwa kufanya kazi kwa umakini

0
1293

Naibu Waziri wa Nishati, – Subira  Mgalu  ameuagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuwa makini katika kupanga vijiji vinavyopaswa kupatiwa huduma ya umeme kwenye wilaya zenye majimbo mawili ya uchaguzi ili kuepusha malalamiko ya kupendelea upande mmoja.

Naibu Waziri Mgalu ametoa agizo hilo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma alipokuwa akikagua miradi ya usambazaji umeme vijijini katika wilaya hiyo yenye majimbo mawili ya Tunduru Kusini na Tunduru Kaskazini.

Amelazimika kutoa agizo hilo baada ya kupata malalamiko kutoa kwa baadhi ya wakazi wa wilaya ya Tunduru waliodai kuwa vijiji vingi vya  jimbo la Tunduru Kaskazini ndivyo vimepatiwa huduma ya umeme huku  jimbo la Tunduru Kusini likiwa na vijiji vichache vilivyopatiwa huduma hiyo.

Naibu Waziri huyo wa Nishati, – Subira  Mgalu  ameelekeza kuwa kazi ya upangaji wa vijiji vilivyo katika mpango wa kupatiwa huduma ya umeme kupitia miradi mbalimbali ishirikishe viongozi wa ngazi tofauti ili kuondoa malalamiko.

Kuhusu kazi ya uunganishaji wilaya ya Tunduru  kwenye umeme wa Gridi ya Taifa,  amesema kuwa wilaya hiyo itaanza kupata  umeme huo kuanzia mwezi Machi mwaka 2019 baada ya kuvuta umeme kutoka wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.

Akiwa wilayani Tunduru, Naibu Waziri Mgalu amewasha umeme katika vijiji vya Namiungo, Mchuluka, Kangomba na Daraja Mbili ambapo kaya zaidi ya mia moja zimeunganishwa na huduma hiyo vikiwemo vituo vya afya na shule.

Wakazi wa vijiji mbalimbali vilivyopatiwa huduma ya umeme wilayani Tunduru wameishukuru serikali kwa kuwafikishia  huduma hiyo ambayo imewawezesha kufanya shughuli za kiuchumi pamoja na kupata huduma za matibabu hata nyakati za usiku tofauti na ilivyokuwa awali.