REA na TANESCO wapewa miezi mitatu kuunganishia wateja Umeme

0
159

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, amewaagiza Watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijjini (REA) kuhakikisha wanawaunganishia umeme wateja wote waliolipia ankara za umeme jijini Mwanza na maeneo ya vijijini ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia leo Desemba 30.

Waziri Kalemani ametoa agizo hilo jijini Mwanza alipokuwa akizungumza na Wafanyakazi wa TANESCO na REA katika kikao kazi cha pamoja.

“Mnataka kila mwananchi awe mita 30 ndipo mumfikishie umeme? Ni kazi yenu kupeleka nguzo hadi muwafikie Wananchi hao. Nisisikie mtu anaongelea suala la mita 30,”amesema Waziri Kalemani.

Waziri Kalemani pia ameiagiza TANESCO kuanzisha madawati ya huduma kwa wateja ili kuhakikisha wateja wanapatiwa huduma bora na kwa wakati ili kuwaondolea adha ya kufuatilia maombi ya kuunganishiwa umeme kwenye Ofisi za TANESCO wilayani.

Aidha, Dkt. Kalemani, amewapongeza Watumishi wa TANESCO kwa utendaji mzuri na kueleza kuwa kwa zaidi ya asilimia 80 utendaji wa TANESCO ni wa Kuridhisha.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi hicho, Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, amewataka Watumishi wote kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri Kalemani, na kueleza kuwa atahakikisha anasimamia na kufuatilia utekelezaji wake kwa ukamilifu.

Kikao kazi baina ya Waziri Kalemani na Watumishi wa TANESCO na REA, ni kikao kazi cha pili baada ya kufanya kikao na Wafanyakazi wa TANESCO mkoa wa Geita wiki iliyopita.