RC Senyamule: Wananchi wenyewe wanataka tuwaweke ndani

0
166

Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema suala la kuwasweka watu ndani wakati mwingine sio la wakuu wa mikoa ama wilaya bali linaombwa na Wananchi kwenye baadhi ya maeneo.

Akihutubia wakati kongamano la Majadiliano ya Ripoti ya Tume ya Haki Jinai linalofanyika katika Chuo cha Mipango mkoani humo Senyamule amesema, baadhi ya maeneo Wananchi wanamfuata mkuu wa mkoa na kumuomba kumkamata mtu fulani ili wapate haki yao.

“Niseme tu kuhusiana na jambo la kuwasweka watu ndani, maana na mimi ni mtuhumiwa. Kuna maeneo Wananchi wanakufuata wanakwambia ukimuweka mtu fulani ndani lazima haki yetu tutaipata kwa hiyo wakati mwingine sio sisi ni Wananchi,” amesema RC Senyamule.

Amefafanua kuwa jambo hilo limekuwa na pande mbili ambapo kuna maeneo wakuu wa mikoa ama wilaya wanawasweka watu ndani lakini kuna sehemu Wananchi wanaamini ili wapee haki basi fulani awekwe ndani.

“Kwenye jamii wapo Wananchi wanakwambia fulani ni mchawi hatumtaki msweke ndani ama uondoke nae hatumtaki kijijini kwetu,” amesema Senyamule.