RC Mbeya atoa saa 24 askari wa TANAPA waliopiga raia wakamatwe

0
412

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ametoa saa 24 kwa Jeshi la Polisi kuwakamata askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wanaotuhumiwa kuwapiga, kuwajeruhi, kuwadhalilisha wananchi pamoja na kupora mifugo yao wilayani Mbarali.

Homera ametoa agizo hilo mara baada ya kukutana na kuzungumza na wananchi ambao wamelalamikia vitendo hivyo vya uvunjifu wa sheria, akisisitiza kuwa Serikali haiwatumi askari wake kwenda kuwapiga wananchi.

“Nimetoa maagizo kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa ahakikishe wale askari wote waliofanya kitendo kama hicho, wakamatwe, wapelekwe polisi na wafunguliwe kesi kama raia wengine. Ninatoa saa 24, askari hao wawe wamekamatwa na wachukuliwe hatua kama wahalifu wengine,” ameagiza Homera.

Awali, taarifa za tukio hilo zilitolewa bungeni jijini Dodoma na Mbunge wa Mbarali Francis Mtega akidai kuwa mbali na wananchi wake kupigwa na kujeruhiwa, wanawake wamevuliwa nguo na kuchomwa kwa mapanga yaliyowekwa kwenye moto pamoja na mbuzi wawili na mbwa watatu kuuawa kwa risasi.

Kufuatia taarifa hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii na uongozi wa TANAPA kufika eneo husika mara moja na kushughulikia tatizo hilo.

Mgogoro huo unahusisha vijiji zaidi ya 30 kuwepo katika eneo la hifadhi ambapo kwa mujibu wa Waziri Mkuu, baada ya mapitio vijiji 27 vilibakishwa kwenye eneo hilo, huku vijiji vitano vilivyokuwa kwenye eneo oevu pindi vitakapovuna mazao yao vinatakiwa vihamishiwe kwenye eneo jingine na wananchi watalipwa fidia.