RC Hapi atwikwa changamoto za Serengeti

0
165

Mbunge wa jimbo la Serengeti, Dkt. Mrimi Amsabi amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Mara Ally Hapi, kuingilia kati na kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakabili wananchi wa jimbo hilo ambazo zimekuwa zikisababishwa na baadhi ya watumishi katika idara mbalimbali.

Dkt. Amsabi ametoa ombi hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Serengeti ikiwa ni sehemu ya ziara ya Mkuu wa Mkoa ya kusikiliza na kutatua kero za Wananchi.

Mbunge huyo amesema kuna baadhi ya watumishi katika idara mbalimbali wameigeuza Serengeti kama genge la kuhujumu na kukandamiza wananchi, hali inayowafanya waione Serengeti kama si mahali salama pa kuishi.

Akitolea mfano kwa Jeshi la Polisi, Mbunge huyo amesema baadhi ya askari wamekuwa wakiwakamata wananchi na kuwabambika kesi hali ambayo inawafanya wananchi kutokuwa na imani na Serikali.

Ameongeza kuwa kuna baadhi ya watumishi wamekuwa wakihujumu miradi ya maendeleo ambayo mingine inatekelezwa kwa nguvu za wananchi, lakini hawaruhusiwi kuhoji chochote huku mapato na matumizi yakiwa ni siri ya watumishi na watendaji wa vijiji na kata.

Mbunge huyo amemuomba Mkuu wa Mkoa kuhakikisha anaingilia kati ili kumaliza changamoto hizo.