RC Geita: Tupande miti kuanzia ngazi ya kaya

0
188

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amewataka wananchi wa mkoa huo kujenga utaratibu wa kupanda miti kuanzia ngazi ya kaya ili kurejesha uoto wa asili ulioanza kupotea.

Akitoa salamu za mkoa huo kwenye hafla ya uzinduzi wa Shamba la Miti Chato mkoani Geita amesema kila kaya ikijenga utaratibu wa kupanda miti, mkoa huo utakuwa na uhakika wa kuwa na miti ya kibiashara na miti ya matunda.

“Tukio hili ni mapinduzi makubwa katika sekta ya uhifadhi mkoani Geita na nina imani huu ni mwanzo wa kurejesha uoto wa asili uliopotea,” amesema Mhandisi Gabriel

Ameongeza kuwa miti ni utajiri na pia ni uchumi hivyo kila mwananchi anapaswa kutumia fursa hiyo kuinua maisha yake.

Hafla ya uzinduzi wa Shamba la Miti Chato ambalo ni la pili kwa ukubwa hapa nchini baada ya lile la Sao Hill, inafanywa na Rais Dkt. John Magufuli.