Rais Samia afungua nyumba 644 Magomeni Kota

0
157

Rais Samia Suluhu Hassan amefungua makazi bora ya nyumba 644 za waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kufungua nyumba hi’zo Rais Samia Suluhu Hassan amesema nyumba hizo ni ahadi ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Dkt. John Magufuli, hivyo atakuwa mstari wa mbele kuendeleza miradi ya watangulizi wake na kutekeleza miradi mipya iliyoahidiwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aidha Rais Samia amesema nyumba hizo hazitokuwa na gharama ya ardhi, bali watalipia nyumba na amewaomba wakazi hao kulipa polepole ili ikifika miaka mitano wawe wamemaliza kulipa.

“Mnaweza kuanza kulipa sasa polepole ili ikifika miaka mitano muwe mmemaliza na ninaomba mnapoishi kwenye nyumba hizi muishi kwa amani na sio mtoto wa mwenzio kakosea basi mnapelekana polisi hapana muishi vizuri.” amesema Rais Samia Suluhu Hassan

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ametoa tathmini ya mradi huo na kusema umegharimu shilingi bilioni 52 hadi kukamilika kwake na kuahidi kutekeleza miradi kama hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tutasimamia miradi kama hii ikamilike kwa wakati na nina ahidi nyumba hizi tutazitunza ili ziweze kudumu.” amesema Profesa Mbarawa