Rais akutana na mtendaji mkuu wa kampuni ya Elsewedy

0
158

Rais Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Elsewedy Electric kutoka nchini Misri, Mhandisi Ahmed El Sewedy, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, Mhandisi El Sewedy amemfahamisha Rais Samia kuwa kampuni yake mbali na kuwa miongoni mwa kampuni zinazojenga mradi wa kuzalisha umeme katika Bwala la Mwalimu Nyerere, pia imewekeza katika miradi mingine na kutarajia kuwekeza zaidi hapa nchini.

Mhandisi El Sewedy amesema kampuni yake inajenga mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 2115 katika Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Pia amesema katika eneo la Kigamboni Jijini Dar es Salaam, kampuni yake imejenga kiwanda cha kuzalisha nyaya za umeme, transfoma, vifaa vya kuzuia nyaya za umeme zisilete hitilafu na mita za umeme, ambacho kinatarajiwa kufunguliwa rasmi mwezi Disemba mwaka 2021.

Aidha, amesema kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yanayoendelea kuwekwa na Serikali, wameamua kuunga mkono na kuwekeza zaidi kwa kujenga eneo la viwanda lenye ukubwa wa mita za mraba milioni mbili ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha mbolea.

Mhandisi El Sewedy ameongeza kuwa anatarajia kuwekeza katika ujenzi wa reli ya kisasa, na katika kipindi cha miaka 2 atahamasisha makampuni takriban hamsini kutoka Misri kuja kuwekeza hapa nchini.

Kwa upande wake Rais Samia amemshukuru Mhandisi El Sewedy na kumhakikishia kuwa Serikali itampa ushirikiano katika kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo kwa muda muafaka.

Rais Samia amesema ujenzi wa eneo maalum la viwanda utasaidia kuchangia kwa kiasi kikubwa utoaji wa ajira na ujuzi.

Aidha, Rais Samia amemjulisha Mhandisi huyo kuwa kwa sasa Tanzania inapitia sheria na sera zake mbalimbali ili kujenga mazingira mazuri zaidi ya biashara na uwekezaji.