Rais : Tutafanya mchujo kwenye majeshi yetu

0
171

Rais Samia Suluhu Hassan amesema wakati umefika wa kuangalia upya mfumo wa utendaji kazi ndani ya majeshi ya Tanzania.

Ametoa kauli hiyo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua ambao ni pamoja na Camilius Wambura aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na Simon Sirro aliyeteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.

Amesema hatua ya kuangalia upya mfumo wa utendaji kazi ndani ya majeshi ya Tanzania utaisaidia nchi kuwa na majeshi imara na yenye nidhamu.

Rais Samia ameongeza kuwa katika siku zijazo mchujo ni lazima ufanyike ndani ya majeshi ya Tanzania, huku lengo kubwa likiwa ni kufanya mageuzi makubwa na kuleta mabadilko ndani ya majeshi hayo.

Wakati wa hafla hiyo amempongeza aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro na kusema kuwa katika kipindi chake amefanya kazi kubwa na nzuri.

Kwa upande wa IGP Wambura, Rais amesema kote alikopita amefanya kazi nzuri na anategemea atafanya kazi nzuri zaidi akiwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini.

Hafla ya kuwaapisha viongozi hao imehudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson.