Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohammed Shein amesema kuwa kongamano la Kiswahili linaloendelea Mjini Zanzibar lina mchango mkubwa katika kuendeleza historia, maendeleo ya kiswahili pamoja na kuitambulisha Zanzibar kimataifa.
Akifungua kongamano la pili la Kimataifa la Kiswahili mjini Zanzibar, Dkt Shein amesema kuwa kongamano hilo linatoa fursa ya kuendeleza uhusiano kati ya wataalamu wa lugha hiyo ya kiswahili popote walipo duniani.
Amesema kuwa Zanzibar inatambulika duniani kote kuwa ndio chimbuko la lugha ya kiswahili fasaha kinachotokana na lahaja ya Kiunguja mjini ambayo ilipitishwa mwaka 1930, hivyo ni vema kongamano hilo likatumika kuiendeleza historia hiyo.
Amesisitiza kuwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume walikuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha lugha ya kiswahili, ndio maana kwa nyakati tofauti lugha hiyo ilitangazwa kuwa rasmi ya Taifa na Zanzibar mwaka 1964, pamoja na lugha ya Taifa la Tanzania mwaka 1967.
Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohammed Shein, ametumia ufunguzi wa kongamano hilo la pili la Kimataifa la Kiswahili, kutoa wito kwa vijana nchini wanaosoma masomo ya kiswahili katika vyuo vikuu mbalimbali nchini kuchangamkia fursa za ajira zilizopo katika nchi za Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Dkt Mohamed Seif Khatib amesema kuwa ni wakati muafaka kwa serikali kusisitiza matumizi fasaha ya lugha ya kiswahili kwa kutambua kuwa ni bidhaa yenye thamani kubwa kiuchumi na kiutamaduni.
Kongamano hilo la pili la Kimataifa la Kiswahili linalofanyika kwa muda wa siku mbili, limeandaliwa na BAKIZA na kushirikisha wataalamu na mabingwa wa lugha ya kiswahili, watunzi wa vitabu, waandishi wa riwaya, tamthilia na mashairi, pamoja na wapenzi wa lugha ya kiswahili kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
