Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) Kristalina Georgieva, kuhusu ushirikiano kati Tanzania na shirika hilo katika masuala ya kiuchumi.
Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa ofisini kwake Ikulu Chamwino mkoani Dodoma amemshukuru Kristalina aliyekuwa nchini Marekani kwa ushirikiano na ufadhili mkubwa ambao IMF umeutoa kwa Tanzania, na amemuhakikishia kuwa Serikali yake itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano huo kwa lengo la kuendelea kujenga uchumi imara wa Tanzania.
Amemueleza juu ya hali ya uchumi wa Tanzania kwa sasa ambapo ukuaji wake umeshuka kutoka wastani wa asilimia 6.9 mwaka 2020 hadi asilimia 4.7 hivi sasa kutokana na changamoto za janga la corona, ambalo limeathiri sekta za uzalishaji na huduma za kijamii zikiwemo utalii, afya na kilimo.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema japokuwa hali ya uchumi wa Tanzania bado ni nzuri, Serikali inahitaji kushirikiana zaidi na IMF kunusuru sekta zilizoathirika na janga la corona na kuendeleza miradi ya kimkakati ambayo utekelezaji wake unaendelea ukiwemo wa ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere katika mto Rufiji utakaozalisha megawati 2,115 za umeme, ujenzi wa reli ya kisasa na ujenzi wa barabara na madaraja.
Amesema pamoja na kukabiliwa na changamoto hizo, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha uchumi ikiwemo kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara kama vile kuondoa dosari za kikodi na ardhi, kuimarisha utawala bora na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Shirika la Fedha Duniani Kristalina Georgieva amempa pole Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha Dkt. John Magufuli aliyekuwa Rais wa Tanzania na amempongeza kwa kupokea kijiti cha Urais.
Amemuhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa IMF ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wake na Tanzania kwa lengo la kuimarisha uchumi.
Kristalina amesema IMF ipo tayari pia kutoa ufadhili wa haraka kwa Tanzania kwa ajili ya kusaidia maeneo yaliyopata madhara makubwa ya kiuchumi kutokana na janga la corona zikiwemo sekta za utalii, afya, uzalishaji na huduma za kijamii na amebainisha kuwa shirika hilo litafanyia kazi mara moja maombi ya mkopo nafuu kutoka Tanzania.
Ameongeza kuwa katika awamu ya pili, IMF imepanga kutumia Dola Bilioni 650 za kimarekani kwa ajili ya kusaidia kwa dharura uchumi wa nchi mbalimbali zikiwemo nchi zinazoendelea zilizopatwa na madhara ya corona.
Kufuatia ahadi hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ambao wamehudhuria katika mazungumzo hayo kukamilisha haraka mchakato wa maandiko ya kuomba mkopo nafuu kutoka IMF ili fedha hizo zisaidie kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za kijamii.