Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa sekta ya Sheria na utoaji wa haki nchini, kuangalia namna bora ya kutayarisha wahitimu na kuongeza maarifa kwa wanasheria walio kazini, yaendane na wimbi la ukuaji wa teknolojia ya habari na Mawasiliano, ili nchi iweze kunufaika na mabadiliko ya teknolojia hiyo.
Rais Samia ametoa wito huo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
“Dunia ipo kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda, ambayo yanaongozwa na sekta ya teknolojia, hivyo Uchumi wa Dunia pamoja na shughuli mbalimbali zinaendeshwa kwa kutumia TEHAMA.”- amesema Rais Samia.
Aidha Rais Samia ameitaka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na vyuo vikuu vyote kuhakikisha kuwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu wanapatiwa ujuzi unaowaandaa kufanya kazi zinazohitaji ujuzi unaolingana na matakwa ya mabadiliko ya Teknolojia.
Hata hivyo Rais Samia amewapongeza viongozi wa sekta ya Sheria kwa hatua wanazochukuwa ikiwemo kutafuta Teknolojia yenye programu za kisasa ambazo zitaimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili.