Rais Samia awataka wazazi kutotupa watoto

0
105

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi na walezi nchini walioshindwa kulea watoto wasiwatupe, na badala yake wawapekele katika vituo vya kulea watoto ili wasaidiwe.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo mkoani Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF).

Ametumia maadhimisho hayo kuwapongeza viongozi wa EOTF chini ya mwenyekiti wake Mama Anna Mkapa kwa kufanya kazi nzuri ya kuwainua wajasiriamali hasa wanawake.

Amesema serikali itaendelea kutatua changamoto za malezi kupitia wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili kuwa na Taifa lenye maadili.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema wanawake wengi wamepata mafunzo ya ujasiriamali baada ya kuwezeshwa na EOTF na kuwataka Watanzania kulinda amani ambayo ni msingi wa mambo mbalimbali.

“Niwakumbushe ndugu zangu Watanzania, mkoa wa Arusha na Zanzibar kwa sasa watalii wameongezeka sana, hii ni baada ya matunda mazuri ya kuitangaza nchi yetu kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour duniani huko. Wajibu wetu ni kulinda amani na utulivu ili watalii na wawekezaji wasiogope kuja nchini” ameongeza Rais Samia Suluhu Hassan

Pia amewakumbusha Watanzania kuendelea kujitokeza kupata chanjo dhidi ya UVIKO – 19 ili kujikinga na maradhi hayo yanayoisumbua dunia.

Aidha, amewataka Watanzania kujiandaa na sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu.