Rais Samia awashushia rungu Askari Polisi

0
345

Rais Samia Suluhu Hassan amemtaka mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IJP) Camillius Wambura kufuatilia matumizi ya fedha wanazokatwa Askari kwa ajili ya Maendeleo, Mfuko wa kufa na kuzikana na fedha nyingine zinazokusanywa na Jeshi hilo.

Rais Samia pia amemtaka IJP wambura kusimamia ufanyaji kazi na uadilifu wa Askari wa Jeshi hilo ili liweze kuwahudumia Wananchi kwa weledi.

Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano wa maafisa waandamizi wa Jeshi la Polisi makao makuu, makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi, Rais Samia amesema Jeshi la Polisi limekuwa likikabiliwa na mambo matatu ambayo ni Rushwa, uzembe na weledi.

Rais amemuagiza IJP Wambura kusimamia yale yote yanayorudisha nyuma utendaji kazi wa Askari wa Polisi ili kuwafanya wawe na ari ya kufanya kazi

Amezungumzia pia suala Polisi kuwabambikia kesi wananchi na kumtaka DCI kupeleleza mashitaka kabla kumkamata na kumsweka mtu ndani.

“DCI kasimamie askari wako wasifanye dhuluma kwa wananchi kwa sababu kumsweka mtu ndani ni mzigo kwa Serikali na kwa familia pia” amesema Rais Samia

Kuhusu Zanzibar, Rais Samia amemtaka IJP kuhakikisha anapeleka Askari wa kulinda maeneo yanayozunguka visiwa hivyo kwani visiwa hivyo ni eneo maalum.

“Zanzibar ni eneo maalum lazima lipewe uangalifu wa kipekee kwa maana ya ujenzi wa nyumba za askari na vitendea kazi lazima na Zanzibar kuwe na bajeti maalum ya kuiwezesha kulinda maeneo yao” amesisitiza Rais Samia

Aidha ameahidi kuwa serikali yake itaendelea kusimamia na kuliwezesha Jeshi hilo kutekeleza majukumu yake ya msingi.