Rais Samia  awaapisha viongozi aliowateua

0
160

Rais Samia Suluhu Hassan amemuapisha Katibu Mkuu Kiongozi, Mawaziri 8 na Naibu Mawaziri 8 ambao aliwateua hapo jana baada ya kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri.

Hafla ya kuwaapisha viongozi hao imefanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Adelardus Kilangi.

Kwanza Rais alimuapisha Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Katanga ambaye pia alikula kiapo cha maadili kwa viongozi.

Mawaziri walioapishwa na Rais Samia ni Ummy Mwalimu ambaye amekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Palamagamba Kabudi – Waziri wa Katiba na Sheria na Mwigulu Nchemba ameapishwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Wengine ni Selemani Jafo ambaye ameapishwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Profesa  Kitila Mkumbo- Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe ameapishwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Balozi Liberata Mulamula kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mohamed Mchengerwa – Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Naibu Mawaziri walioapishwa ni William Ole Nasha aliyeapishwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Abdallah Ulega kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mwita Waitara kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Pauline Gekul ameapishwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Wengine walioapishwa ni Mhandisi Hamad Masauni aliyeapishwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mbarouk Nassoro Mbarouk kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mwanaidi Ally Hamis kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Hamad Hassan Chande ameapishwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.