Rais Samia ateuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya GCA

0
140

Rais Samia Suluhu Hassan ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kituo cha Dunia cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi (Advisory Board of the Global Centre on Adaptation – GCA).

Taarifa ya uteuzi huo iliyowasilishwa na Ban Ki-moon, Mwenyekiti wa Bodi ya GCA na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, ilitangazwa wakati wa mkutano kando ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Nairobi, Kenya.

Uteuzi huo ni utambuzi wa wazi wa uongozi imara wa Rais Samia katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi siyo tu katika eneo la Afrika bali pia kimataifa. Tanzania imekuwa ikiongoza katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mabadiliko ya tabianchi barani Afrika.

Mbali na Rais Samia, wajumbe wengine wa Bodi hiyo ni Rais wa Senegal, Macky Sall, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Akinumwi Adesina, na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), Kristalina Georgieva.

Kituo cha Dunia cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi (GCA) ni taasisi kubwa kabisa duniani inayojikita katika kusimamia masuala ya uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi. Mpaka sasa, GCA imeweza kufanikisha upatikanaji wa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 50, na Tanzania iko mstari wa mbele kupokea faida za fedha hizo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.