Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa mchakato wa katiba mpya ni wa Watanzania wote na sio wa wanasiasa kama ambavyo baadhi ya watu wanadhani, na kwamba uandaaji wake unahitaji muda wa kutosha na ushiriki wa makundi yote.
Rais Samia ametoa rai hiyo wakati akifungua mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa na Wadau wa Demokrasia Kutathmini Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi na Hali ya Siasa Nchini unaofanyika kwa siku tatu kuanzia leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Katiba si mali ya vyama vya siasa. Katiba ni mali ya Watanzania, awe na chama au hana. Hivyo, matengenezo yake yanahitaji tafakuri sana,” amesema Rais Samia.
Ameeleza kuwa bado Watanzania wengi hawaifahamu katiba ya sasa, wengine wakidhani ilani ya CCM ndio katiba, na kwamba Serikali inatekeleza mchakato wa kutoa elimu kwa umma ili waifahamu katiba ya sasa, waweze kutoa maoni sahihi pindi watakapotakiwa kufanya hivyo.
Wakati huo huo, amesisitiza kwamba ruhusa ya kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa iliyotolewa sio tiketi ya kuvunja sheria za nchi kama ambavyo inafanyika sasa na baadhi ya vyama.
Hata hivyo Rais Samia ameongeza kuwa hashangazwi na hilo kutokea kwa sababu baadhi ya vyama havina ajenda ya kueleza Wananchi.
“Tulianza, ooh na katiba, tukaenda ikakatika katikati, bandari, sasa imekatika tumerudi tena katiba,” ameeleza Rais Samia akitolea mfano namna baadhi ya vyama vinavyoruka kutoka ajenda moja kwenda nyingine.
Ametahadharisha kuwa, hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria, na kwamba yeyote atakayekiuka sheria atachukuliwa hatua bila muhali, huku akiongeza kuwa Watanzania wote ni sawa, na kwamba hakuna Mtanzania bora zaidi ya mwingine.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) Profesa Ibrahim Lipumba alimpongeza Rais Samia kwa hatua za kuimarisha demokrasia anazochukua huku akipendekeza maeneo manne kufanyiwa maboresho kwenye katiba ya sasa kabla ya chaguzi za mwaka 2024 na mwaka 2025.