Rais wa Tanzania ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan amesema kifo cha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhandisi Elias Kwandikwa, kimeacha pengo kubwa kwa serikali kwani alikuwa kiongozi mwadilifu na anayependa kujifunza kila siku.
“Kifo cha Kwandikwa kimeacha pengo sio tu kwa familia bali pia kwenye serikali, hadi mauti yanamkuta alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, hivyo ni wazi kifo chake ni pigo kwa serikali,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema kipindi akiwa Makamu wa Rais, marehemu Elias Kwandikwa alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na walifanya kazi kwa karibu hasa walipokuwa na ziara katika mikoa mitatu.
“Tulianza Singida, tukaenda Tabora, tukamalizia Shinyanga, katika ziara hiyo alikuwa makini na mfuatiliaji, mtulivu na msikivu na asiye na makuu, hakuwahi kutoa sababu ya kutoka nje ya ziara mpaka tumemaliza,” ameongeza Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema sababu hizo zilipelekea yeye (Rais Samia) na Hayati Dkt. John Magufuli kumteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na mwaka 2020 kuteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
“Kutokana na sifa hizo hizo ndio zilizonipelekea kumpa dhamana ya kuongoza wizara nyeti ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,” amesema Rais.
Waziri Elias Kwandikwa alifariki dunia Agosti 2, 2021 jijini Dar es Salaam na atazikwa kijijini kwao Ushetu, Kahama Agosti 9 mwaka huu.