Rais Samia Suluhu Hassan amesema kila kiongozi anapaswa kufanya kazi kwa bidii katika eneo lake, huku akikemea tabia ya kudharauliana kati ya Mawaziri na Naibu Mawaziri, jambo linalokwamisha ufanisi wa kazi.
Ameonya kuwa Waziri yeyote ama Katibu Mkuu mwenye tabia ya kujikweza ataondolewa katika wadhifa wake, kwa kuwa haendani na kasi anayoitaka.
Rais Samia Suluhu Hassan amempongeza Katibu Mkuu Kiongozi aliyemuapisha hii leo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma Balozi Hussein Katanga ambaye katika hotuba yake mara baada ya kuapishwa alieleza kuwa kazi za Serikali zinapaswa kufanywa kwa ushirikiano, jambo ambalo kwa sasa halipo.
Amemuagiza Balozi Katanga kutatua tatizo hilo la kutokuwepo kwa ushirikiano kwenye utekelezaji wa masuala mbalimbali ya Serikali, kwa kuwa katika maeneo yote aliyowahi kufanya kazi aliweza kufanikisha jambo hilo.
Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo katika hotuba yake mara baada ya kumuapisha Katibu Mkuu Kiongozi, Mawaziri 8 na Naibu Mawaziri 8 aliowateua hapo jana.