Rais Magufuli kutekeleza ahadi ya Dkt Kikwete

0
218

Rais John Magufuli ambaye yuko njiani kuelekea mkoani Shinyanga, amewaomba Wakazi wa Shelui mkoani Singida walioomba kujengewa Kituo cha Afya kuwa wavumilivu, na kwamba ifikapo mwezi Januari mwaka 2020 Serikali itawapelekea Shilingi Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo mara baada ya Mkazi mmoja wa eneo hilo kumuomba kuwasaidia ujenzi huo ulioshindwa kutekelezwa kwa takribani miaka 15, huku akikumbushia ahadi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt Jakaya Kikwete aliyoitoa ya kuwapelekea Shilingi Milioni 200 kwa ajili ya ujenzi huo.

Akijibu ombi hilo, Rais Magufuli amesema kuwa, ahadi ya Rais Mstaafu Kikwete ni ahadi ya Serikali, hivyo ataitekeleza na kuongeza Shilingi Milioni 50 nyingine.

“Ahadi ya Rais Mstaafu Kikwete mimi nitatekeleza kama kijana wake ambaye pia aliniamini na kuniteua katika nafasi mbalimbali, hivyo msiwe na wasiwasi”, amesisitiza Rais Magufuli.

Amezitaka kampuni zote zitakazoshinda zabuni kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hicho cha afya cha Shelui, kutekeleza ujenzi huo kwa uaminifu na kwa haraka, ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa urahisi.