Rais John Magufuli amesisitiza kuwa ataendelea kuwatumikia Watanzania wote bila ya kujali tofauti zao za dini, ukabila na vyama.
Rais Magufuli ameyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya chuo cha ualimu Tarime mkoani Mara, ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani humo.
Amesema kuwa ataendelea kuwatembelea Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini badala ya kusafiri nje nchi, lengo likiwa ni kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Rais Magufuli amewashauri wakazi hao wa Tarime kutoingiza masuala ya kisiasa katika shughuli za maendeleo, kwani kwa kufanya hivyo ni kuchelewesha maendeleo.
Pia ameahidi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Tarime ikiwa ni pamoja na ile ya afya, maji na barabara ili kuwaondolea adha inayowakabili wakazi wa wilaya hiyo.
Wakati wa mkutano huo, Rais Magufuli ameahidi kutoa Shilingi Bilioni Moja nukta Tano kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Rorya.