Rais Magufuli kuchukua fomu ya uteuzi wiki hii

0
274

Rais wa Tanzania ambaye pia ni mgombe wa Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) atachukua fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi hiyo wiki hii jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema kuwa siku ya kiongozi huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kuchukua fomu hiyo itatangazwa.

“Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu John Pombe Joseph Magufuli… atachukua fomu wiki hii,” amesema Polepole.

Akidokeza kuhusu namna chama hicho kimejipanga kuingia kwenye siasa za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu, Polepole amesema watafanya siasa bora zaidi kuwahi kuwepo tangu enzi za Mwalimu Nyerere, na wana uhakika wa kushinda kwani wanaingia kwenye uchaguzi wakiwa na mtaji wa wapiga kura milioni 16.8 ambao ni wanachama wa chama hicho.

Wakati huo huo amesema kuwa Agosti 15 ndani ya Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kutakuwa na tamasha kubwa la ndani ambapo chama hicho kitakutana na wasanii zaidi ya 109 na shughuli kubwa kuzindua nyimbo za chama zitakazotumika kabla, wakati na baada ya kampeni.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefungua pazia la wagombea walioteuliwa na vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu kuchukua fomu za kugombea ambapo tayari baadhi ya wagombea wa vyama mbalimbali wamefika kwenye ofisi za NEC zilizopo jijini Dodoma kuchukua fomu.