Rais Magufuli azungumzia alama za taifa

0
1617

Rais Dkt. John Magufuli ameagiza bendera, nembo na wimbo wa taifa kuendelea kutumika kama ilivyokuwa awali.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu jijini DSM imesema Rais MAGUFULI ameagiza kutumika kwa alama hizo za taifa kama ilivyokuwa kabla ya kuandikwa kwa barua ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwezi uliopita kwenda kwa wakuu wa vyuo na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Rais MAGUFULI amesema maelekezo yaliyotolewa katika barua hiyo yanaathiri uzalendo wa Watanzania na inaleta mkanganyiko wa tafsiri ya rangi na alama zilizomo katika bendera ya Taifa.

Amesema tangu anasoma shule hadi leo anafahamu Bendera ya Taifa ina rangi ya njano na sio rangi ya dhahabu, na rangi hiyo ya njano inawakilisha madini yote, sio dhahabu peke yake.

Rais MAGUFULI amesisitiza kama kuna mabadiliko ni lazima yafanyike kwa kuzingatia taratibu kwa kuwa jambo hilo ni la Kitaifa.

Ametoa wito kwa watanzania kuendelea kuwa wazalendo, kuipenda nchi yao na kuitangaza popote walipo ilimradi wanazingatia sheria na maslahi ya Taifa.

Barua iliyoandikwa Novemba 23 mwaka huu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia baada ya kupokea maelekezo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliagiza kutumika kwa rangi ya dhahabu katika bendera ya taifa badala ya rangi ya njano.