Rais Dkt. John Pombe Magufuli amerejea kauli yake ya kuwataka Watanzania kutokuwa na hofu kubwa dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) na badala yake waendelee kuchukua tahadhari kama zinavyoelekezwa na wataalamu.
Rais ametoa kauli hiyo wakati akimuapisha Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, hafla iliyofanyika wilayani Chato, mkoani Geita.
Amefafanua kuwa kumekuwa na upotoshaji mkubwa ambao unasambazwa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii na kusababisha hofu kubwa kwa wananchi, hali ambayo haisadii kupunguza tatizo bali kuliongeza na kutengeneza sintofahamu kubwa.
Amewataka Watanzania wote hasa wanasiasa pamoja vyombo vya habari kuacha kueneza taarifa zinazowajaza watu hofu ama kutumia ugonjwa huu kwa manufaa ya kisiasa na badala yake waungane kutoa elimu sahihi na kuhimizana kuchukua tahadhari za kutoambukizwa.
Ameelezea kushangazwa kwake na viongozi ambao wanazuia watu wanaofariki dunia kusafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani kwao, na Viongozi wa Dini walioonesha kutetereka kiimani, hivyo ametoa wito kwa viongozi wote kusimama imara, kuonesha uongozi wa kweli na kuwapa matumaini wananchi badala ya kuwajaza hofu.
Katika uapisho huo, Rais Magufuli amemtaka Nchemba kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake Marehemu Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga aliyefariki dunia tarehe 01 Mei, 2020 na pia kushirikiana na viongozi wenzake katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali.
“Nimekuteua kwa mara ya pili kwa sababu naamini unaweza kutekeleza jukumu hili vizuri, na bahati nzuri vijana wengi niliowateua hawajaniangusha, kwa hiyo nakutakia heri katika kazi zako na Mungu akutangulie,” amesema Rais Magufuli.