Rais Magufuli awatoa Watanzania hofu ya Corona

0
306

Rais Dkt John Magufuli amewataka watanzania kuendelea kuchapa kazi huku wakiendelea kuchukua tahadhari na kujifukiza ili kujikinga na ugonjwa Corona.

Rais Magifuli pia ametaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutokubali kila chanjo inayoletwa hapa nchini bila kuwa na uhakika nayo.

Akihutubia wananchi katika kijiji cha Butengo wilayani Chato katika hafla ya uzinduzi wa shamba la miti Silayo, Rais Magifuli amesema, hana mpango wa kutangaza kufungia watu ndani kutokana na tishio la maambukizi ya ugonjwa wa corona na kuwataka Watanzania kuchapa kazi.

Aidha amewataka wananchi wasitishike na maneno kuwa corona itarejea tena kwani tayari Mungu yupo pamoja na watanzania.

“Ndugu zangu nawasihi tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya corona na tujifukize lakini tuchape kazi, tusitishike na Corona na wala hakuna chanjo yoyote tusihangaike tutaletewa magonjwa tusiyoyajua,” amesema Rais Magufuli

Siku za hivi karibuni kumekuwa na jumbe kwenye mitandao ya kijamii ikiaminisha wananchi kuwa ugonjwa wa corona umerejea tena hapa nchini.