Rais Magufuli awataka Watanzania kuendelea kumtegemea Mungu

0
375

Rais Dkt John Magufuli leo ameungana na Waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Imakulata Chamwino mkoani Dodoma kusali Misa Takatifu ya Krismasi ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Baada ya Misa hiyo iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Paul Mapalala, Rais Magufuli amewapongeza na kuwatakia heri Watanzania wote kwa sikukuu ya Krismasi na amewataka kuendelea kumshukuru Mungu kwa miujiza na upendo mkubwa anaolitendea Taifa la Tanzania.

Amesema upendo na miujiza ya Mungu kwa Tanzania inajidhihirisha katika kipindi hiki ambapo dunia inapita katika wakati mgumu wa janga la ugonjwa wa Corona ambapo maelfu ya watu wanaendelea kupoteza maisha kila siku, lakini Tanzania imeepushwa na janga hilo na maisha ya Watanzania yanaendelea kama kawaida.

Rais Dkt Magufuli amewaomba Watanzania wote waendelee kumshukuru na kumuomba Mungu aendelee kulilinda Taifa lao dhidi ya ugonjwa huo na kuwaombea Wananchi wa Mataifa mengine waepushwe na Corona.

Ametoa wito kwa Viongozi wa Mataifa mbalimbali duniani kukubali kumweka Mungu mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona badala ya kutegemea nguvu za binadamu pekee.

Pamoja na kuwatakia heri ya Krismasi Watanzania, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kujenga Taifa lao pamoja na kuhakikisha wanamtanguliza Mungu kwa kila jambo.