Rais Magufuli atoa wito kwa mabalozi wawakilishi nchini

0
347

Rais Dkt. Magufuli amepokea hati za utambulisho za mabalozi watatu walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Mabalozi waliowasilisha hati hizo ni Regine Hess, Balozi wa Jamhuri ya Ujerumani, Hussein Bin Ahmed Mohamed Ibrahim Al-Homaid, Balozi wa Taifa la Qatar, na Ahmed Djellal, Balozi wa Algeria.

Akizungumza na mabalozi hao Rais Magufuli amewakaribisha hapa nchini na kuwahakikishia kuwa serikali inadhamiria kuukuza na kuuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na nchi hizo.

Rais Magufuli ametoa wito kwa mabalozi hao kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali kutoka nchi zao kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali hasa kilimo, mafuta, gesi, viwanda na madini kwa kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali za kutosha katika sekta hizo ambazo zinahitaji ushirikiano wa pamoja katika uwekezaji.

Aidha, amewaomba mabalozi hao kufikisha shukrani zake kwa viongozi wa nchi zao na kuwakaribisha kutembelea Tanzania kwa ziara rasmi ama kutembelea vivutio vingi vya utalii vilivyopo.

Kwa upande wao, Mabalozi hao wamemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali kuwapokea na katika kipindi cha uwakilishi wao wameahidi kufanya juhudi za kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano hasa katika masuala ya kiuchumi ambayo serikali inayapa kipaumbele.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Watu wa Algeria nchini Mhe. Ahmed Djellal kwenye hafla
iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo jioni Jumanne Januari 14,
2020
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya
Shirikisho la Ujerumani nchini Mhe. Regina Hess kwenye hafla
iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo jioni Jumanne Januari 14,
2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule Taifa la Qatar
nchini Mhe. Hussein Bin Ahmed Mohamed Ibrahim Al-Homaid katika hafla
iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo jioni Jumanne Januari 14,
2020