Rais Magufuli atoa maagizo ya kumaliza migogoro ya ardhi Morogoro

0
255

Rais John Magufuli ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Morogoro uhakikishe mashamba yaliyofutwa hati zake yanagawiwa kwa wananchi ili wayatumie kwa kilimo ili kumaliza migogoro ya ardhi katika mkoa huo.
 
Rais Magufuli ametoa agizo hilo katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa mahandaki ya reli ya kisasa (SGR) kutoka Morogoro hadi Makutupora pamoja na mradi wa barabara.

Akizungumzia mradi huo wa reli ya kisasa Rais Magufuli amebainisha kuwa zaidi ya shilingi trilioni 6 zinatumika katika ujenzi wake. Mahandaki aliyoyawekea jiwe la msingi yapo manne na yote kwa pamoja yana urefu wa zaidi ya kilometa mbili

Katika hatua nyingine Rais amesema haridhishwi na kasi ya wakandarasi wazalendo kwa kushindwa kutekeleza miradi wanayopatiwa kwa wakati, hivyo amewataka wabadilike.

Awali, akiwa njiani kuelekea wilayani Kilosa mkoani humo amemuagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ndani ya siku saba awasilishe kwake hati za shamba alilopewa muwekezaji raia wa China lenye ukubwa wa takribani hekta 5,000, ili sehemu ya shamba hilo ifutwe na kugawiwa kwa wananchi.

Hatua hiyo imetokana na malalamiko ya wananchi waliyoyatoa kwa Rais Magufuli aliposimama kuzungumza nao, ambao wamelalamikia kitendo cha kukodishwa mashamba na muwekezaji badala ya kuwa na mashamba yao binafsi