Rais Magufuli ateua CAG, Balozi, Kamishna wa Kazi na Majaji 12

0
249

Rais John Magufuli amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali ambapo Charles Kichere ameteuliwa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kichere anachukuwa nafasi ya Profesa Mussa Juma Assad ambaye kipindi chake cha miaka Mitano katika nafasi hiyo kinakwisha kesho Novemba Nne.

Kabla ya Uteuzi huo Kichere alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imewataja wengine walioteuliwa kuwa ni
Katarina Revocati anayekua Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe na kabla ya uteuzi huo alikuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

Rais Magufuli amemteua Mhandisi Aisha Amour kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, ambapo kabla ya Uteuzi huo, alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Kanali Francis Mbindi yeye ameteuliwa kuwa Kamishna wa Kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Gabriel Malata ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.

Aidha Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Majaji 12 wa Mahakama Kuu, ambapo walioteuliwa ni
Dkt Zainabu Mango aliyekua Wakili wa Serikali Mkuu katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Edwin Kakolaki ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa katika Ofisi ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya Nchini na Dkt Deo Nangela ambaye
kabla ya uteuzi huo alikuwa katika Ofisi ya Tume ya Ushindani.

Majaji wengine ni Kapela Manyanda aliyekuwa katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Elizabeth Mkwizu ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Augustine Rwizile aliyekuwa Naibu Msajili wa Mahakama na Ephery Sedekia aliyekuwa Katibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya uteuzi huo.

Majaji wengine wa Mahakama Kuu walioteuliwa na Rais Magufuli ni Angaza Mwaipopo ambaye alikuwa
Ofisi ya Rais, Ikulu,
Joachim Tiganga ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Kassim Robert aliyekuwa
katika Ofisi ya Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu cha Wizara ya Fedha na Mipango , Said Kalunde ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Angela Bahati ambaye alikuwa Katibu Msaidizi wa Tume ya Kurekebisha Sheria.

Wateule wote pamoja na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna Watano wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambao waliteuliwa hivi karibuni, wataapishwa kesho Novemba Nne saa Tatu na Nusu asubuhi, Ikulu jijini Dar es salaam.